| Chapter 7 |
1 |
"Msiwahukumu wengine, msije nanyi mkahukumiwa na Mungu;
|
2 |
kwa maana jinsi mnavyowahukumu wengine, ndivyo nanyi mtakavyohukumiwa; na kipimo kilekile mnachotumia kwa wengine ndicho Mungu atakachotumia kwenu.
|
3 |
Kwa nini wakiona kibanzi kilicho jichoni mwa ndugu yako, na papo hapo huioni boriti iliyoko jichoni mwako?
|
4 |
Au, wawezaje kumwambia ndugu yako, `Ndugu, ngoja nikuondoe kibanzi jichoni mwako`, wakati wewe mwenyewe unayo boriti jichoni mwako?
|
5 |
Mnafiki wewe! Ondoa kwanza boriti iliyoko jichoni mwako na hapo ndipo utaona waziwazi kiasi cha kuweza kuondoa kibanzi kilichoko jichoni mwa ndugu yako.
|
6 |
"Msiwape mbwa vitu vitakatifu wasije wakageuka na kuwararua ninyi; wala msiwatupie nguruwe lulu zenu wasije wakazikanyaga.
|
7 |
"Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtapata; bisheni, nanyi mtafunguliwa.
|
8 |
Maana, aombaye hupewa, atafutaye hupata, na abishaye hufunguliwa.
|
9 |
Je, kuna yeyote miongoni mwenu ambaye mtoto wake akimwomba mkate, atampa jiwe?
|
10 |
Au je, akimwomba samaki, atampa nyoka?
|
11 |
Kama basi ninyi, ingawa ni waovu, mwajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, hakika Baba yenu wa mbinguni atafanya zaidi: atawapa mema wale wanaomwomba.
|
12 |
"Watendeeni wengine yale mnayotaka wao wawatendee ninyi. Hii ndiyo maana ya Sheria ya Mose na mafundisho ya manabii.
|
13 |
"Ingieni kwa kupitia mlango mwembamba. Kwa maana njia inayoongoza kwenye maangamizi ni pana, na mlango wa kuingilia humo ni mpana; waendao njia hiyo ni wengi.
|
14 |
Lakini njia inayoongoza kwenye uzima ni nyembamba, na mlango wa kuingilia humo ni mwembamba; ni watu wachache tu wanaoweza kuigundua njia hiyo.
|
15 |
"Jihadharini na manabii wa uongo. Wao huja kwenu wakionekana kama kondoo kwa nje, lakini kwa ndani ni mbwa mwitu wakali.
|
16 |
Mtawatambua kwa matendo yao. Je, watu huchuma zabibu katika miti ya miiba, au tini katika mbigili? La!
|
17 |
Basi, mti mwema huzaa matunda mema, na mti mbaya huzaa matunda mabaya.
|
18 |
Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mema.
|
19 |
Kila mti usiozaa matunda mema utakatwa na kutupwa motoni.
|
20 |
Kwa hiyo, mtawatambua kwa matendo yao. ic
|
21 |
"Si kila aniambiaye, `Bwana, Bwana,` ataingia katika Ufalme wa mbinguni; ila ni yule tu anayetimiza mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.
|
22 |
Wengi wataniambia Siku ile ya hukumu: `Bwana, Bwana! kwa jina lako tulitangaza ujumbe wako, na kwa jina lako tuliwatoa pepo na kufanya miujiza mingi.`
|
23 |
Hapo nitawaambia: `Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni mbele yangu, enyi watenda maovu.`
|
24 |
"Kwa sababu hiyo, kila mtu anayeyasikia maneno yangu na kuyazingatia, anafanana na mtu mwenye busara, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba.
|
25 |
Mvua ikanyesha, mito ikafurika, pepo kali zikavuma na kuipiga nyumba hiyo. Lakini haikuanguka kwa sababu ilikuwa imejengwa juu ya mwamba.
|
26 |
"Lakini yeyote anayesikia maneno yangu haya bila kuyazingatia, anafanana na mtu mpumbavu aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga.
|
27 |
Mvua ikanyesha, mito ikafurika, pepo kali zikavuma na kuipiga nyumba hiyo, nayo ikaanguka; tena kwa kishindo kikubwa."
|
28 |
Yesu alipomaliza kusema maneno hayo, umati wa watu ukashangazwa na mafundisho yake.
|
29 |
Hakuwa kama walimu wao wa Sheria, bali alifundisha kwa mamlaka.
|